Share news tips with us here at Hivisasa

Baraza la Maimam na Wahubri nchini, CIPK, limewakashifu wanaotumia vazi la buibui kutekelezea maovu hususan katika Kaunti ya Mombasa.

Kulingana na katibu mtendaji wa baraza hilo Sheikh Mohammed Khalifa, katika siku za hivi majuzi, vazi hilo limekuwa likitumika kutekeleza visa vya ugaidi na uhalifu.

Katika mahojiano na mwandishi huyu mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Sheikh Khalifa alisema kwamba ni kinyume na misingi ya dini ya Kiislamu kwa vazi kama hilo la heshima kutumika katika maovu.

Khalifa alisema kwamba kuna baadhi ya wanawake wanojihusisha na ukahaba wakilitumia vazi hilo nyakati za usiku na kuwaonya kutolidhalilisha vazi hilo.

Aidha, amewasihi Waislamu kuwakosoa hadharani wale wanaovunja heshima ya vazi hilo na kusema kwamba dini haijaruhusu mwanamke yeyote kulitumia vazi la heshima kutenda maovu kwa kisingizio cha kutafuta mahitaji ya kimsingi.

“Tunawaomba maafisa wa polisi kuwatia nguvuni wanaotumia vazi la buibui kufanya maovu. Tunaomba wafunguliwe mashtaka kwa sababu wanadhalilisha vazi la heshima, lililoteuliwa na mwenyezi mungu kumstiri mwanamke,” alisema Khalifa.

Hapo awali Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Nelson Marwa aliwaonya wanaotumia vazi hilo la buibui kutekeleza uhalifu na visa vya ugaidi kwamba watakabiliwa kikamilifu.