Share news tips with us here at Hivisasa

Muungano wa upinzani wa Cord umekashifiwa vikali na baadhi ya viongozi kutoka kaunti ya Nakuru, kwa kuendesha siasa za mgawanyiko ambao adhari zake katika ngazi ya mashinani zinaweza kugeuka na kuwa za kikabila.

Ni baada ya chama cha Wiper, moja kati ya vyama vinavyounda Cord, kuwaondoa wabunge watatu kwenye kamati mbalimbali za bunge Jumatano, ambao inabashiriwa wamekuwa wakiunga mkono uongozi wa Jubilee, na kuwa fuko wa serikali kwenye upinzani.

Watatu hao ni ikiwemo Regina Ndambuki wa eneo bunge la Kilome, John Munuve wa eneo bunge la Mwingi Kaskazini na Joe Mutambo wa Mwingi ya Kati.

“Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, aongoze chama kwa namna ya kuwapa viongozi wengine uhuru wa kutangamana na serikali kwa faida ya Mwananchi kimaendeleo. Viongozi wote ni sharti waungane, utengano wa vyama na siasa hautasaidia Kenya,” alisema Paul Chebor, MCA Solai.

Viongozi wanastahili kuwa mfano mwema kwa ‘Wanjiku’ mashinani, utengano huo bungeni ni picha isiyostahili kuonyeshwa mlipa kodi maskini,” alisema mwakilishi wa wadi ya Visoi Edward Gitau.

Jumanne ODM chama tanzu cha Cord pia, kiliwatimua wabunge James Momanyi wa Bobasi, Khatib Mwashetani wa Lunga Lunga na George Olum wa Lang’ata ambao walikuwa wanachama wa kamati ya kuratibu shughuli za bunge (HBC).