Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Viongozi wa mrengo wa upinzani wamewaagiza wafuasi wao kutoka mtaa wa Kibera haswaa vijana kujisajili kwa kiasi kikubwa kama wapiga kura ikizingatiwa kuwa usajili huo wa wapiga kura utang'oa nanga siku ya Jumatatu.

Wakizungumza walipozuru mtaa wa Kibra siku ya Jumamosi viongozi hao wamesema kuwa tume huru ya kusimamia uchaguzi na kuratibu mipaka IEBC ina njama ya kusajili wapiga kura wengi kwa maeneo ambayo ni ngome kuu ya chama cha Jubilee.

Akiwahutubia wakaazi kwenye hafla hiyo ya kisiasa iliyoandaliwa katika ukumbi wa Laini Saba katika mtaa wa Kibera, kinara wa Cord Raila Odinga aliukashifu mrengo tawala wa Jubilee kwa usemi kuwa ulitumia miradi iliyofeli ya huduma za vijana kwa taifa NYS ili kuwapotosha wapiga Kura.

Raila aidha amewaomba wakaazi wa Kibera kuuunga mkono mrengo wa Cord haswa kwenye uchaguzi wa mwaka 2017 ili kuwezesha mrengo wa Cord kutawala nchi ya Kenya kwani utaleta mabadiliko makubwa.

"Jubilee ilitumia miradi ya NYS ambayo kwa sasa imefeli ili kuwadanganya wakaazi wa Kibera kwa kuwafumba macho ndio wawapigie kura. Nawaomba mjisajili kama wapiga kura kwa wingi na mutuunge mkono kwenye uchaguzi ujao na tukiingia kwenye ikulu na kuongoza taifa hili tutawaletea mabadiliko makubwa," alisema Raila alipokuwa akiwahutubia wakaazi.

Akiongea katika mkutano huo pia, gavana wa kaunti ya Nairobi Evans Kidero alisisitiza kuwa ushindi wake kuwa gavana wa Nairobi ulikuwa wa haki na hakuhonga mtu yeyote katika kesi iliyowasilishwa mahakamani na mheshimiwa Ferdnand Waititu. 

Kidero alisema kuwa madai hayo ni propaganda za mrengo wa Jubilee na hazitamshtua kisiasa.