Dereva jasiri aliyekuwa akisafirisha bidhaa za elekroniki kwenye barabarabara ya Naivasha-Mai Mahiu, alilikabili vikali kundi la wezi wa kupora magari barabarani katika kisa ambacho kimemiminiwa sifa tele japo alibaki na majeraha.
Tukio hilo lilifanyika usiku wa kuamkia Jumatatu karibu na kituo cha kibiashara cha Chechinia wakati dereva huyo aliyekuwa akielekea nchi jirani ya Uganda kutoka Mombasa alipata barabara imefungwa kwa gari ndogo aina ya Salon.
Adam Mwaura, aliyeshuhudia kisanga hicho, alisema kwamba watu wawili waliokuwa wamevalia ‘mavazi ya mwitu’ walikimbilia trela hilo ili kulipora, kabla ya kumwamrisha dereva kutoka nje lakini akakaidi.
“Wezi hao walimshambulia dereva huyo lakini akapigana nao wawili kijasiri huku akijaribu kuendesha gari na kupiga honi kuashiria hatari. Walimkata kwenye kichwa na mikono kwa silaha butu,” alisema Mwaura.
Hali hiyo ilivutia madereva wengine wa malori ya masafa marefu ambao waliharakisha kwenda kumsaidia mwenzao aliyekuwa amefaulu kuendesha gari majangili hao wakiwa bado ndani.
“Washukiwa hao wawili walifaulu kuruka kutoka kwa lori na kuingia gari lao na kutoroka wakiwa wanne,” alisema.
Afisa mmoja wa polisi wa ngazi ya juu aliyeomba kubanwa jina amedhibitisha hayo akisema dereva huyo ametibiwa na kuruhusiwa kuondoka hospitali baada ya kuandikisha ripoti.
Wizi unaohusisha magari ya masafa marefu umekuwa ukiongezeka kwenye barabara hiyo huku madereva wakidaiwa kushirikiana na wezi kupora bidhaa hizo.