Dereva wa trela na utingo wake wameponea kifo baada ya gari lao kushika moto karibu na eneo la Salgaa siku ya Jumatatu.
Trela hilo lilikuwa linasafirisha betri kutoka Uganda kuelekea Mombasa wakati ajali hiyo ilipotokea.
Dereva wa trela hilo Wanyama Bilali, alisema magurudumu ya nyuma ya lori hilo yalishika moto baada yake kufunga breki kwa ghafla.
Kwa muujibu wake, aliona moshi ukitoka kwenye magurudumu hayo ya nyuma, hatua iliyompelekea kusimama.
“Nilikuwa nikitoka Uganda nikielekea Mombasa. Nikiwa kwenye mteremko wa kuelekea Salgaa, nikaona magurudumu ya nyuma yakiwa yameshika moto. Hapo niling’ang’ana hadi nikatoa sehemu ya mbele ya trela hiyo. Tulijaribu kuzima moto huo lakini tukashindwa lakini wazima moto walifika baadaye na kutusaidia.
Akidhibitisha kisa hicho, OCPD wa Rongai Joseph Mwamburi alisema kwamba dereva huyo alifanikiwa kutenganisha sehemu ya mbele na ile ya nyuma ya lori hilo kabla ya waliokuwa karibu kumsaidia kuuzima moto huo.
OCPD huyo alidokeza kuwa hakuna aliyejeruhiwa kwenye tukio hilo la saa kumi na mbili asubuhi.
“Nilielezwa kuwa dereva alimuona msichana mdogo akijaribu kuvuka barabara na hapo akafunga breki kwa ghafla, hatua iliyopeleklea magurudumu ya nyuma kushika moto. Hata hivyo kwa bahati nzuri, wapita njia walimsaidia dereva na utingo wake kutenganisha sehemu ya mbele na ile ya nyuma, na hakuna aliyejeruhiwa,” alisema Mwamburi.
Mwamburi alisema kuwa idadi ya ajali za barabarani katika barabara hiyo ya kuelekea Salgaa imepungua kutokana na uwepo wa matuta na ishara za barabarani, shughuli ambayo imeendelezwa na mamalaka ya usafiri na usalama wa barabarani NTSA.
Trela hilo lilipelekwa katika Kituo cha polisi cha Salgaa.