Licha ya kuwa taifa la Kenya liko na sheria madhubuti ya kuzuia dhulma za kijinsia, bado visa vingi vya unyanyasaji wa jinsia vinaonekana kuongezeka.
Haya ni kwa mujibu wa mratibu wa muungano wa mashirika ya Pwani ya kutetea dhulma za kijinsia Betty Sharon, ambaye ameongeza kuwa wahusika wakuu hawatekelezi majukumu yao ipasavyo huku ufisadi nao ukichangia kuachiliwa kwa washukiwa
Akiongea mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Sharon alisema kuwa vitengo vya kushughulikia dhulma za kijinsia katika vituo vya polisi vinakumbwa na matatizo huku wengi waliopo katika vitengo hivyo wakiwa hawana ufahamu wa kutosha wa kushughulikia maswala ya dhulma za kijinsia.
Itakumbukwa kuwa visa vya dhulma za kijinsia vimezidi kuongezeka hasa katika mahakama ya Mombasa, huku ikiwa kisa cha hivi juzi, Ijumaa iliyopita, jamaa mmoja alifikishwa mahakamani kwa kumnajisi binti wa miaka kumi na miwili na kisha kumuua katika eneo la Likoni.
Katika kesi hiyo, koti iliamuru kufanyiwa uchunguzi wa akili kwa mshukiwa na mwili wa marehemu kufanyiwa upasuaji.