Mwenyekiti wa tume ya maadili na kupambana na ufisadi nchini (EACC), Philip Kinisu amekiri kuwa tume hiyo ilifanya kosa ilipomuondolea lawama aliyekuwa waziri wa ugatuzi, Anne Waiguru.
Akizungumza mbele ya kamati ya maswala ya kisheria katika bunge la kitaifa siku ya Jumatano,Kinisu alisema kuwa hatua hiyo ilitokana na ukosefu wa mawasiliano kati ya tume hiyo na sekta mbalimbali za serikali.
‘‘Uchunguzi uliopelekea Waiguru kuondolewa lawama ulifanywa kwa upande mmoja huku ule wa kutaka kujua jinsi milioni sh791 zilivyotumika ukifanywa na sekta nyingine ya serikali,’’ alisema Kinisu.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa tume hiyo imeweza kurejesha mali ya takriban bilioni sh9 kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita ikiwemo pesa taslimu milioni sh600. Aliongeza kuwa hatua ya kubuniwa kwa wakala wa urejesho wa mali imesaidia pakubwa kurejesha mali iliyopotezwa kwa njia ya ufisadi.
Hata hivyo, Kinisu aliongeza kuwa taifa ya Uingereza limekubali kurejesha milioni sh51, mali iliyonyakuliwa na kampuni za Uingereza zilizopatikana na hatia ya kuwahonga maafisa wa Kenya ili kupata kandarasi kutoka kwa baraza la mtihani nchini na pia tume ya uchaguzi na uratibu wa mipaka nchini IEBC.
EACC ilikuwa inaijulisha kamati ya maswala ya kisheria katika bunge la kitaifa kuhusu majukumu ambayo tayari yametekelezwa na tume hiyo na changamoto inazopitia tume hiyo wakati inapotekeleza majukumu yake.