Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Huku taifa la Ufaransa likiomboleza kufuatia mashambulizi ya kigaidi ambayo yaliwaua zaidi ya watu 130, Kaunti ya Mombasa itakuwa miongoni mwa maeneo na Kaunti ambazo zitafaidi na mpango wa serikali wa kuimarishwa kwa usalama na maafisa wa usalama.

Kulingana na naibu wa inspekta mkuu wa polisi nchini Samuel Arachi, maeneo yote ambayo yamekuwa na visa vya kudorora kwa usalama na kulengwa na magaidi kama vile miji ya Mombasa, Nairobi, na maeneo ya Kaskazini mwa Kenya yataongezewa maafisa kuweka doria ili kuzuia nafasi yoyote ya magaidi na wahalifu

Arachi alisema kuwa vikosi vyote vya usalama tayari vinaendelea kufanya mazoezi ili kutoa msaada wa kiusalama katika maeneo yanayoaminika kukubwa na uhalifu, ambapo aliwataka wananchi kusaidia kupigana na ukosefu wa usalama na kuboresha zaidi.

Naibu inspekta mkuu huyo alikuwa akiongea katika hafla moja ya kufuzu kwa maafisa wa polisi, ambapo aliahidi kuwa serikali, kupitia idara ya usalama itaendelea kukazana kila kukicha ili kuhakikisha kuwa wananchi na nchi kwa ujumla iko na usalama wa kutosha.

Eneo la Pwani kwa jumla limekuwa na visa vya vijana kushawishiwa na kujiunga na makundi ya kigaidi, na kwa miaka mitatu ikifuatana magaidi wa Al shabaab yamekuwa yakiwalenga maafisaa wa usalama pamoja na raia kwa kile kinachoaminika kuwa uwepo wa jeshi la Kenya katika nchi ya Somalia.