Kwa mara nyingine tena maskwota waliokabidhiwa hati miliki katika shamba la Waitiki lililoko Likoni, Mombasa, wamehimizwa kutii agizo la Rais Uhuru Kenyatta linalowataka kulipia ada ya umiliki wa shamba hilo. 

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Msemaji wa Ikulu Manoah Esipisu amewashahuri maskwota hao kulipuzilia pendekezo la baadhi ya viongozi wa kisiasa wanaotaka serikali kuu kuyasimamia malipo hayo kwani anasema njia ya pekee itakayowawezesha wakazi hao kumiliki ardhi hiyo kikamilifu ni kujilipia. 

''Rais alisema, na ni wazi kwamba ili mfaidike na shamba hilo lazima mgharamike. Kwa hivyo nawasihi mfuate agizo la Rais, shamba liwe lenu,'' alisema Esipisu. 

Esipisu alikuwa akizungumza katika Ikulu ya Mombasa siku ya Jumatano alipoandaa kikao na wanahabari. 

Siku ya Jumamosi wikendi iliyopita, Rais Kenyatta, aligawa hati miliki takribani 5,000 kwa maskwota wanaoishi katika shamba lenye utata la Evanson Waitiki, na kuwaagiza kulipa shilingi 1,000 kila mwezi kwa kipindi cha miaka 12 kama ada ya umiliki. 

Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa kisiasa mjini Mombasa akiwemo mwakilishi wa wanawake Mishi Mboko, wameitaka serikali kuipunguza ada hiyo kwa madai kuwa baadhi ya wakazi hawana uwezo wa kuilipia.