Share news tips with us here at Hivisasa

Familia moja iliyopatwa na mkasa wa moto ulioteketeza nyumba yao Jumamosi katika kituo cha kibiashara cha Maili Kumi, imepokea wa kifedha ili kuwawezesha kuanzisha upya maisha yao.

Mwakilishi wa wadi hiyo ya Bahati katika bunge la kaunti ya Nakuru Peter Nderitu, aliongoza wanabiashara, machifu, viongozi wa kidini na wakaazi katika hafla ya kuchangisha fedha za kumjengea upya makaazi Jane Gathoni mama wa watoto watatu, ambapo jumla ya shilingi elfu 80 zilichangishwa.

Katika hafla hiyo ya Ijumaa, pia familia hiyo ilipokea msaada wa vyakula na malazi, ikizingatiwa hamna kilichookolewa kwenye mkasa huo wa moto.

“Mtu hatoi msaada kwa sababu ni tajiri, ila ni kwa sababu ya utu,” Nderitu alisema.

“Ningetaka kuhimiza ushirikiano ambao nimeona hapa leo udumu katika wadi hii. Undugu, umoja na ushirikiano utatuwezesha kupigana na mikasa mbali mbali inayotokea,” Nderitu aliongeza.

Viongozi wa makanisa mbalimbali waliombea eneo la mkasa ili kufukuza ‘mapepo’ yanayoaminika kusababisha moto huo kwenye boma mbili tofauti zilizo karibu, katika muda wa siku mbili.