Familia moja kutoka Likoni, Mombasa, sasa inaitaka serikali kuiharakisha shughuli ya kuitambua miili ya wanajeshi waliowawa katika shambulizi la Al Shabaab nchini Somalia.
Familia hiyo inadai kuishi kwa hofu baada ya kuarifiwa kua mwanao ni miongoni mwa wanajeshi wa KDF waliohangamia katika shambulizi lilotekelezwa na wanamgambo wa Al Shabaab katika kambi ya wanajeshi wa muungano wa Afrika katika eneo la El Adde Somalia mapema mwezi huu.
Kwa mujibu wa mmoja wa familia hiyo, mwanao alikuwa miongoni mwa wanajeshi waliopelekwa Somalia, na tangu shambulizi hilo, juhudi zao za kutaka kuwasiliana naye hazijafua dafu kwani hapatikani kwa simu.
Kwa sasa wanaitaka serikali kuiharakisha shughuli ya kuitambua miili hiyo ili waweze kuifahamu hatima ya mwanao.
Hata hivyo, serikali hadi sasa haijatoa taarifa kamili kuhusu idadi ya wanajeshi waliouawa katika shambulizi hilo, ila inazidi kusafirisha hadi Nairobi kutoka Somalia miili ya waliohangamia pamoja na manusura.