Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mali ya kiwango cha thamani kisichojulikana imeteketea katika mtaa wa YMCA viungani mwa mji wa Nakuru Jumanne usiku, na kupelekea familia moja kulala nje kwa baridi.

Akidhibitisha kisa hicho, naibu wa OCPD wa Nakuru Janet Wasige ameeleza ya kwamba moto huo ulianza mwendo wa saa moja usiku wa Jumanne wakati ambapo mwenye nyumba hiyo na familia yake hawakuwa nyumbani.

Kadhalika, Wasige ameongeza ya kwamba mwenye nyumba hiyo alikuwa ameenda dukani hatua chache na nyumba hiyo, na aliporejea akapata nyumba hiyo inateketea.

Ingawa majirani na wasamaria wema walijaribu kuuzima moto huo, jitihada zao ziliambulia patupu kwani moto huo uliwazidi, na kupelekea kutafuta usaidizi wa zima moto, ambayo ilifika muda mfupi baada ya kuitwa mahala hapo, na kusaidia moto huo usisambae katika nyumba jirani.

Wasige amebaini kuwa hakuna kilichookolewa kutoka mkasa huo, ambao uliteketeza nyumba hiyo ya zaidi ya vyumba vitatu.

Ijapokuwa hakuna mtu yeyote aliyepoteza maisha kutokana na moto huo, maswali mengi yanazidi kuibuliwa jinsi moto huo ulivyoanza, kwani hakukua na shuguli yoyote ya upishi ilikuwa inaendelea nyumbani humo.

Hata ingawa chanzo cha moto huo bado hakijabainika kwa sasa, mwenye nyumba ametoa wito kwa serikali ya kaunti na wasamaria wema kumsaidia yeye.