Baadhi ya wakaazi mjini Mombasa wamelazimika kulala nje baada ya nyumba zao kufurika maji kufuatia mvua kubwa inayoendelea kunyesha tangu siku ya Jumapili.
Familia nyingi katika maeneo ya Magongo na Bokole katika eneo la Changamwe, yale ya Bangladesh, maeneo ya Mishomoroni na Bombolulu huko Kisauni yameathirika pakubwa na mvua hiyo inayoendelea kunyesha mjini Mombasa.
Wakaazi hao aidha wameitaka Serikali ya Kaunti ya Mombasa kuizibua mitaro ya maji taka ili kukabiliana na mafuriko ambayo yanashuhudiwa mjini Mombasa.
Kitengo cha kukabiliana na majanga katika Kaunti ya Mombasa kupitia kwa mkuu wake Anthony Njaramba aliyezungumza na wanahabari siku ya Jumatatu, alisema kwamba kitengo hicho kiko makini kuzikabili dharura za aina yoyote zitakazochangiwa na mvua hiyo.
"Kitengo chetu cha kukabiliana na majanga kiko nyanjani kuzikabili changamoto zinazotokana na mvua hiyo ili kuona kwamba wakaazi wetu wako salama na hawakumbwi na changamoto, japo twajua ni vigumu kwa baadhi ya wakaazi kuyahama maeneo yao lakini tunawasihi kuzingatia maagizo ili kuepukana na majanga," alisema Jaramba.
Hata hivyo, Shirika la Msalaba Mwekundu katika Kaunti ya Mombasa halijatoa takwimu zozote rasmi kuhusiana na mvua hiyo japo Maafisa wa Shirika hilo wamo nyanjani kuitathmini hali hiyo huku mvua ikiendelea kunyesha kwa siku ya tatu mtawalia.