Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mashirika ya kutetea haki za kibinadamu yamesema hayaridhishwa na hukumu ya miaka saba iliyopewa maafisa wawili wa polisi waliomuua mtoto wa miaka 14.

Akizungumza siku ya Jumatatu, Mkurugenzi mkuu wa shirika la Muslims for Human Rights (Muhuri) Khelef Khalifa, alisema maafisa hao walifaa kufungwa maisha wala sio miaka saba.

Khelef, alisema kuwa mashirika hayo yatazidi kuwatetea wananchi wanaopitia mateso kutoka kwa maafisa wa polisi nchini.

Kwa upande wake, Francis Auma, afisa katika shirika la Haki Africa, alisema kutolewa kwa hukumu hiyo kutatoa ujumbe mkali kwa maafisa wa polisi wanaojihusisha na mauaji ya kiholela nchini.

Wakati huo huo, Umazi Zani, mamake mwendazake Kwekwe Mwandaza, alipinga hukumu hiyo na kusema kuwa ni ndogo mno ikizingatiwa walipoteza mtoto wao ambaye hawatampata tena maishani.

Upande wa washtakiwa ukiongozwa na wakili wao Gerald Magolo, uliomba washtakiwa hao waachiliwe huru kwa dhamana wakijiandaa kukata rufaa.