Kufuatia kuendelea kupanuka na kuongezeka kwa idadi ya watoto wa mtaa, mkurugenzi mkuu wa elimu katika Kaunti ya Mombasa Abdikadir Kike amesema serikali ina mpango wa kuwapa jamii hiyo elimu.
Aidha Kike amewataka kina mama ambao wana watoto walio na umri wa kuenda shule pamoja na wale ambao walifikia darasa la nane na kidato cha nne kuenda katika shule ya Boston, iliyoko katika gereza kuu la Shimo la Tewa, ili kupata mafunzo ya kosi mbali mbali.
Akiongea mjini Mombasa siku ya Jumatatu, mkurugenzi huyo alisema nafasi ipo kwa wale ambao walimaliza darasa la nane la kuendeleza masomo yao katika shule hiyo kitengo cha sekondari, na kuhakikisha kuwa wanakamilisha masomo ya kidato cha upili na kufanya taaluma wanazoazimia maishani.
Kike aliwashauri wazazi wote katika mitaa yote ya kaunti hiyo ya Mombasa kuchukua jukumu la kutembelea shule hiyo na kuwapa nafasi wanao kuendeleza ndoto yao kimasomo, na kusema kuwa kila mtoto anayo haki ya kupata elimu kwa mujibu wa katiba ya Kenya.
“Kama kuna vijana au wazazi wana watoto wa kuenda shule nawashauri wafanye hima waende kwenye shule ya Boston ambayo huwashughulikia wananchi wale ambao hawana uwezo wa kifedha kupata elimu, na kufanya taaluma mbali mbali,” Kike alisema.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa shule hiyo hutoa masomo bila malipo na kuna kosi mbali mbali zinazowafaa vijana kama vile uhandisi, useremala na taaluma nyinginezo.