Share news tips with us here at Hivisasa

Visa vya watoto pamoja na kina mama ambao hawana makao kunajisiwa na vijana katika jiji la Mombasa vimeongezeka katika siku za hivi majuzi.

Kulingana na jamii hiyo ambayo haina makazi maalumu na ambayo hutumia uga wa umma wa Makadara katika shughuli zao za kuombaomba hela kutoka kwa wapiti njia, kwa nyakati za hivi karibuni, baadhi ya kina mama pamoja na watoto wa kike wamekuwa wananajisiwa na wale wa kiume kulawitiwa na vijana, hususani wale wakutumia dawa za kulevya.

Familia hizo zaidi ya ishirini kupitia kwa mama Jamila Chengo kwenye mahojiano na mwandishi huyu siku ya Jumanne, walisema kuwa wengi wao hujipata katika hali hiyo kwa kupuliziwa dawa, hasa nyakati za usiku wanapokuwa wamelala, na wanapoinusa dawa hiyo huwa wanakosa fahamu na kujipata siku ya pili wakiwa wamenajisiwa na hata kuibiwa pesa na baadhi ya chakula na bidhaa nyinine ambazo wanakuwa nazo.

“Siku nyingi tulikuwa tunalala katika nyumba za Municipal ambazo hazikuwa na watu lakini tangu tutolewe huwa tunalala katika mahali hapa pa uga huu wa Makadara, au wengine huelekea uko ufuoni na kujitafutia mahali pa kuweka angaa kichwa, na ni hatari kwa sababu mna mateja wengi ambao sisi kina mama tunaweza kunajisiwa na hata kuuliwa,” alisema Chengo.

Serikali ya kaunti imekuwa ikisema mara nyingi kuwa inatafuta suluhu la kuwahamisha wahusika kutoka katikati ya jiji na kutafutiwa njia mbadala, lakini hadi wakati huu jamii hiyo inaendelea kuongezeka kila mara.