Gavana wa Kaunti ya Nyamira John Nyagarama amesema kuwa serikali yake imeweka mikakati kuhakikisha kuwa viwango vya elimu katika kaunti ya Nyamira vinaimarika hata zaidi.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Akihutubia washikadau mbalimbali wa sekta ya elimu kwenye hafla yakupokeza shule mbalimbali za umma vitabu, kwenye uwanja wa Shule ya msingi ya Nyamira siku ya Jumanne, Gavana Nyagarama alisema kuwa serikali yake ina mipango yakuhakikisha kuwa shule zote za umma kwenye kaunti hiyo zina bidhaa zakutosha.

Aidha, alisema kuwa serikali ya kaunti inanuia kujenga maktaba ya umma Nyamira.

"Ninapenda sana maswala ya elimu na ndio maana serikali yangu imeweka mikakati kuhakikisha kuwa shule zote za umma zina bidhaa za kutosha. Ingawaje majukumu haya yanastahili kutekelezwa na serikali ya kitaifa, mimi niko tayari kuwarai wawakilishi wadi kuunga mkono azma yangu yakujenga maktaba kwenye shule mbalimbali humu Nyamira," alisema Nyagarama.

Gavana Nyagarama alisema kuwa kamwe serikali yake haitoketi nakuangalia viwango vya masomo vikiendelea kudorora katika kaunti ya Nyamira, huku akiwahimiza viongozi mbalimbali wa kisiasa kushirikiana na serikali yake ili kubaini changamoto zinazokumba shule mbalimbali za umma katika eneo hilo.

"Elimu ni muhimu sana kwa mataifa yanayostawi na kwa kweli tutatia juhudi kwa kuhakikisha kuwa shule zetu zina bidhaa zakutosha, na pia tutawasaidia wanafunzi werevu kutoka familia maskini na ufadhili wa kimasomo. Ninawaomba viongozi mbalimbali katika kaunti hii kushirikiana na serikali yangu kutambua changamoto shule mbalimbali zinazokumbana nazo ili kutafuta mbinu yakutatua changamoto hizo," alisema Nyagarama.