Gavana wa kaunti ya Nyamira John Nyagarama amesema serikali yake imetoa magari ya kaunti ili kushirikiana na yale ya maafisa wa polisi kuimarisha hali ya usalama katika kaunti hiyo katika msimu huu wa sherehe za krismasi.
Kulingana na gavana huyo, magari ya polisi hayawezi tosha kufanya patroli katika sehemu zote za kaunti na hivyo kuongeza magari ya kaunti ili kushirikiana kuimarisha usalama kwa wakazi wote.
Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumanne mjini Nyamira, gavana Nyagarama alisema serikali yake iko tayari kushirikiana na polisi kuhakikisha hali ya usalama imeimarishwa kikamilifu.
“Mimi kama gavana wa kaunti hii nafurahi wakati nasikia hakuna kisa chochote cha ualifu kimetendeka hapa Nyamira,” Nyagarama alisema.
“Serikali yangu tayari imetoa magari ili kushirikiana na yale ya polisi na maafisa hao wayatumie kuleta na kuimarisha usalama hadi msimu huu wa sherehe ukamilike,” aliongeza Nyagarama.
Aidha, gavana aliwataka madereva wa magari na waendesha bodaboda kuwa waangalifu ili kupunguza visa vya ajali barabarani .
“Naomba kila mwendeshaji awe mwangalifu barabarani katika sekta ya uchukuzi,”Nyagarama alisema.