Gavana wa Kaunti ya Nyamira John Nyagarama amejitokeza kuwasihi wakaazi kuthibiti viwango vya mahindi na maharagwe wanavyoiuzia bodi ya kitaifa ya nafaka NCPD.
Nyagarama alisema kuwa serikali ya kaunti hiyo haijaafikia vilengo vya kuzalishaji nafaka ya kutosheleza mahitaji ya kaunti.
Akihutubia wakazi wa Riamanoti kule Borabu siku ya Jumanne, Gavana Nyagarama aliwahimiza wakaazi hao kuthibiti uuzaji wa nafaka kwa bodi hiyo kwa kuwa huenda janga la njaa likaikumba kaunti ya Nyamira.
Aliongezea kwa kuwahimiza wazazi ambao wamekuwa wakiendesha biashara hiyo kwa minajili ya kuwalipia wanao karo ya shule kutafuta mbinu mbadala za kufadhili masomo ya watoto wao.
"Nimekuwa nikipata ripoti kuwa baadhi yenu mmekuwa mkiuza nafaka kwa bodi ya nafaka nchini NCPD na hilo kamwe halitaruhusiwa kwa maana sisi wenyewe kama kaunti hatujatosheleza mahitaji yetu. Nawahimiza wazazi kujisajili kupata ufadhili wa kimasomo almaarufu basari ili kuwawezesha wanao kupata masomo," alisema Nyagarama.
Nyagarama aidha aliwaonya vikali wakazi wa eneo hilo dhidi ya kushirikiana na madalali wanao nunua nafaka zao kwa bei ya chini na kisha kuziuza kwa bei ya juu kwa NCPB.
Gavana huyo alisema kuwa hali hiyo huenda ikailazimu iadara ya kilimo katika kaunti hiyo kuanzisha mpango wa kununua nafaka kutoka kwa wakulima ili kuzihifadhi kwa matumizi ya siku za usoni.
"Ikiwa kwamba lazima muuze nafaka basi nawaomba mungoje hadi pale serikali yangu kupitia kwa idara ya kilimo itakapoanzisha mpango wa kununua nafaka hizo kutoka kwenu, kwa maana tungependa kuzihifadhi kwa matumizi ya siku za baadaye," aliongezea Nyagarama.