Gavana wa kaunti ya Mombasa Hassan Ali Joho amefanya mabadiliko katika baraza la mawaziri pamoja na baadhi ya maafisa wakuu katika serikali hiyo.
Aliyekuwa waziri wa Ardhi, Nyumba na Mipango Francis Thoya sasa ndiye katibu wa serikali ya kaunti, huku waziri wa Kilimo, Uvuvi na Ufugaji Anthony Njaramba akiteuliwa kushikilia wadhfa huo wa idara ya ardhi.
Khamis Mwaguya, aliyekuwa katibu wa serikali ya kaunti amehamishwa hadi afisa mkuu wa wafanyikazi katika afisi ya gavana, huku aliyekuwa akishikilia wadhfa huo Khamis Juma akihamishwa kuwa mshirikishi wa usimamizi wa kaunti ndogo.
Aliyekuwa waziri wa utalii Joab Tumbo amehamishwa hadi nafasi mpya iliyobuniwa ya mshauri wa miradi ya maji, usalama na mabadiliko ya hali ya anga.
Abdalla Mwabami, aliyekuwa afisa mkuu katika idara ya vijana, michezo na jinsia na mwenzake Simon Mbaru wa idara ya utalii na tamaduni wamepewa likizo.
Aidha, Rabia Salim na Rajab Idd Babu ndio wameteuliwa kushikilia idara hizo mbili mtawalia.
Gavana Joho alisema siku ya Alhamisi kuwa mabadiliko hayo ni katika hali ya kuboresha huduma kwa wananchi wa kaunti ya Mombasa huku akiahidi mabadiliko zaidi.