Gavana wa Kaunti ya Nakuru Kinuthia Mbugua ameahidi kufadhili miradi mbalimbali ya vijana huku akilenga kuwaimarisha maishani.
Akizungumza kupitia mtandao wake wa Facebook siku ya Ijumaa alipotembelewa na kundi la vijana la Toupe Redspaxx, Mbugua alisisitiza umuhimu wa kuwapa vijana nafasi ya kujitegema wenyewe.
“Serikali yangu itakuwa imara kufadhili miradi ambayo vijana watazindua. Nawarai vijana wajitokeze na miradi yoyote ile ambayo inanuia kuimarisha maisha yao,” alisema Mbugua.
Kundi hilo la Troupe Redspaxx ambalo hukuza talanta za vijana wanaocheza na kusakata densi katika kaunti hiyo pia inaanda tamasha ya kutambua vijana wenye talanta ambayo inatarajiwa kuandaliwa November 5 kwenye hoteli ya Eldorado.
Mbugua pia alichukua fursa hiyo kuwapa fedha za kufadhili tamasha hiyo huku akielezea umuhimu wa kukuza vipaji na talanta mbalimbali miongoni mwa vijana.
“Vijana wanapaswa kupewa nafasi sawa katika maendeleo nchini ili wapate nafasi ya kukuza talanta zao. Wengi wameweza kujikimu kutokana na talanta zao zikiwemo ucheshi, kuimba, na densi, hivyo basi ni jambo la kutilia maanani,” alisema Mbugua.