Gavana wa Kaunti ya Nakuru Kinuthia Mbugua ameapa kupigana dhidi ya dhuluma ya jinsia katika kaunti hiyo.
Akizungumza siku ya Alhamisi ofisini mwake alipotembelewa na mwenyekiti wa tume ya taifa ya jinsia na usawa Winfred Lichuma, Mbugua alitaja tendo hilo kama kikwazo katika maendeleo nchini.
“Serikali yangu itakuwa imara kuhakikisha dhuluma za jinsia zinakabiliwa vilivyo katika kaunti hii na kote nchini kwa jumla,” alisema Mbugua.'
Lichuma alisema visa vya dhuluma ya jinsia vinaendelea kukithiri, huku akiongeza kuwa Nakuru ni kaunti ya tatu kuanzisha kampeni hiyo.
“Azma yetu ni kuungana na serikali ya taifa na za kaunti kupigana na dhuluma ya jinsia katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya polisi na afya,” alisema Lichuma.
Mbugua pia alipongeza juhudi za tume hiyo katika kueneza umoja na usawa miongoni mwa jinsia.
“Tume hii imechukua hatua kubwa katika kutatua shida za jinsia na za usawa nchini tangu kuzinduliwa chini ya katiba mpya. Tutaungana nao kuhakikisha usawa katika sekta zote kaunti hii,” aliongeza Mbugua.
Gavana huyo pia alisema kuwa kuimarisha maisha ya akina dada itakuwa nguzo muhimu katika kupigana na vita hivyo vya jinsia.