Gavana wa kaunti ya Nakuru Kinuthia Mbugua anataka sekta ya elimu kuwekwa kwenye mfumo wa ugatuzi kama njia moja ya kuangazia changa moto zinazokabili sekta hiyo.
Mbugua alisema shida nyingi zikiwemo kuwepo kwa miundo msingi duni zinaweza kutatuliwa pekee ikiwa elimu itagatuliwa kikamilifu na wala si ilivyo kwa sasa ambapo ni ile ya chekechea ambayo imo mikononi mwa serikali za ugatuzi.
“Ikiwa elimu itagatuliwa, maswala ya walimu yanafaa kusalia na tume ya kuwaajiri waalimu ambayo ina mipango mwafaka ya kuwakagua kwa kina,”Mbugua alisema.
Gavana huyo aliyasema hayo baada ya kutoa blanketi na magodoro kwa wanafunzi wa shule ya upili ya wavulana ya Mai Mahiu kufuatia mkasa wa moto uliochoma bweni moja mwaka wa 2015.
Akiwahutubia wakazi wa eneo hilo, Mbugua pia alimzomea mwenyekiti wa mamlaka ya NACADA John Mututho kwa kufanya kampeni licha ya kuwa mfanyikazi wa serikali.
Naye naibu wake Joseph Ruto alisema kuwa Mututho amefeli kwenye kazi zake na anafaa kuachishwa kazi ili ipewe wakenya walio na nia ya kuifanya.