Share news tips with us here at Hivisasa

Gavana wa Nakuru Kinuthia Mbugua amesema kwamba vita dhidi ya pombe haramu ni wajibu wa kila mtu, na sio tu wa serikali pekee.

Amesema hayo alipokuwa akizungumza katika wadi ya Kabatini iliyo kwenye kaunti ndogo ya Bahati Alhamisi alipozuru eneo hilo kukagua miradi ya maendeleo, ambapo ilibainika kuwa maeneo kadhaa ya wadi hiyo yangali yanakumbana na tatizo la uwepo wa pombe haramu.

"Kila mtu anafaa kuelewa kuwa ni jukumu la wote katika Jamii; wakubwa kwa wadogo kukabiliana na pombe haramu. Hatungependa kurejea katika siku ambazo watu walipoteza maisha kutokana na pombe hiyo haramu ambayo inaweza kukabiliwa watu wanapoungana," alisema gavana huyo.

Wakati huo huo, amethibitisha kuwa serikali ya kaunti ya Nakuru itajibidiisha hata zaidi kukabiliana na pombe hiyo haramu.

Huku akifungua rasmi miradi kadhaa ya maji kama vile bwawa la shule ya upili ya Heroes na lile lilo katika eneo la Kamugima kwenye wadi hiyo inayotarajiwa kufaidi wakazi 3,500 wa eneo la Kabatini na viungani mwake, gavana aliashiria kuwa serikali ya kaunti imejitolea kukabiliana na shida ya maji.

"Uhaba wa maji ambao umekuwa ukishuhudiwa katika eneo hili utazikwa kwenye kaburi la sahau. Tunapanua mradi wa kusambaza maji kwa shule na hata kwenye makazi ya watu, lengo letu likiwa kuhakikisha kila mtu anapata maji safi ya kutumia kila wakati," aliashiria gavana Mbugua.

Kwa upande mwingine, amewataka wakazi wa wadi hiyo kupanda miti katika msitu wa Dundori ambao umeathiriwa pakubwa na ukataji wa miti, akithibitisha kuwa serikali ya kaunti itafanya kazi pamoja na wakazi kuurejesha msitu huo katika hadhi yake ya hapo awali.

"Kufikia sasa kuna zaidi ya madereva 50 waliohitimu kutoka kwa wadi hii. Nawahimiza vijana hao kutumia leseni walizopata kumudu mahitaji yao ya kila siku kwa kujipatia fedha. Siso sisi wote tunaoweza kwenye vyuo vikuu, lakini kupitia kwa mafunzo tunayopata katika vyuo vya mafunzo anuwai na taasisi zinazotoa mafunzo mbalimbali, tunaweza kumaliza ukosefu wa ajira," alisema gavana.

Kando na miradi hiyo ya maji, gavana pia alizindua mradi wa taa za barabarani eneo Kabatini, shule ya chekechea ya Nyathuna na kituo cha kiafya cha Kabatini Health Centre.

Gavana alikuwa ameandamana na mawaziri mbalimbali wa serikali ya kaunti ya Nakuru pamoja na maafisa wengine wa serikali yake.