Gavana wa kaunti ya Nyamira John Nyagarama amewasihi wahisani kujitokeza ili kusaidia kufadhili masomo ya wanafunzi werevu wanaotoka katika familia maskini.
Akihutubu wakati wakushuhudia rasmi hafla ya benki ya KCB kuwapa ufadhili wanafunzi waliofanya vyema kwenye mtihani wa darasa la nane KCPE mwaka jana, Gavana Nyagarama alisema kuwa kuna idadi kubwa ya wanafunzi werevu ambao hawawezi pata nafasi ya kuelimika kwa sababu ya umaskini.
"Ni ombi langu kwa wahisani kujitokeza kufadhili masomo ya wanafunzi werevu wanaotoka katika familia maskini kwa kuwa idadi kubwa ya wanafunzi hawa huachwa nje kutokana na ufadhili wa mashirika mbalimbali, hali ambayo huchangia pakubwa katika kuzima ndoto zao," alisema Nyagarama.
Nyagarama aidha aliongeza kusema kuwa serikali yake ina mipango ya kuzindua rasmi hazina itakayo wasaidia wanafunzi maskini katika jamii kupata elimu.
"Serikali yangu ina mipango ya kuzindua hazina itakayowasaidia wanafunzi maskini kupata ufadhili wa kimasomo, na zoezi hilo litaanza hivi karibuni baada ya bunge la kaunti ya Nyamira kuliidhinisha," aliongezea Nyagarama.