Gavana wa kaunti ya Nyamira John Nyagarama aliongoza hafla ya uzinduzi wa usambazaji vyandarua vya kuzuia mbu elfu 481,637 nje ya majengo ya afisi kuu za kaunti ya Nyamira. 

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Akihutubu kwenye hafla hiyo, Nyagarama amesema asilimia 75 ya wakazi wa kaunti hiyo wamo kwenye hatari ya kuambukizwa malaria, na amewahimiza wananchi waliojisajili kupokea vyandarua vya kuzuia mbu kutembelea vituo vilivyo karibu nao ili kupokezwa vyandarua vyao shughuli anayosema itatamatika Jumatatu wiki kesho. 

"Asilimia 75 ya wakazi wa kaunti hii wamo kwenye hatari ya kuambukizwa ugonjwa wa malaria ila nawahimiza wananchi waliojisajili kupokea vyandarua hivyo vya kuzuia mbu kutembele vituo vya usambazi neti vilivyo karibu nao ili kupokezwa vyandarua vyao kwa kuwa shughuli hiyo itatamatika jumatatu wiki ijayo," alisema Nyagarama. 

Kwa upande wake, kamishna wa kaunti hiyo Josphine Onunga aliwahimiza wakazi wa kaunti hiyo kutumia vyandarua hivyo kwa kujikinga kutokana na mbu badala ya kutumia vyandarua hivyo kusitiri mboga shambani. 

"Ningependa kuwahimiza wakazi kutumia vyandarua hivi kwa kujikinga kutokana na mbu badala ya kuvitumia kusitiri mboga shambani," aliongeza Onunga. 

Aidha, afisa wa shirika la usambazaji vyandarua hivyo nchini Anthony Okoth alisema kuwa tayari shirika hilo limesambaza takriban vyandarua elfu 950 kwenye kaunti ya Kisii, na sasa anatarajia kuwa watafanikiwa kusambaza zaidi ya vyandarua elfu 400 kwenye kaunti ya Nyamira. 

"Tayari tumesambaza vyandarua elfu 950 kwenye kaunti ya Kisii, na tunatarajia kuwa tutafanikiwa kusambaza vyandarua zaidi ya elfu 400 huku Nyamira," alisema Okoth.