Huduma za umeme kwenye gereza kuu la Naivasha pamoja na makaazi ya askari wa kulinda gereza hilo zimekatizwa, kutokana na deni la shilingi milioni sita.
Hatua hiyo imeibua wasi wasi na hofu ya kiusalama kwenye gereza hilo lenye zaidi ya wafungwa elfu tatu wengi wao wakiwa washukiwa hatari kwa usalama.
Pia gereza ndogo ambalo husheheni wafungwa walio na vifungo vilivyo chini ya miaka mitano, pia limekatiwa umeme.
Sasa usalama umeimarishwa ndani na nje ya gereza hilo kuu la Naivasha, ambapo wafungwa wa vifungo vya maisha na wizi wa kimabavu hupelekwa.
Afisa mkuu msimamizi wa gereza hilo Patrick Mwenda amedhibitisha hayo, akisema shirika la usambazaji umeme nchini (KP) lilichukua hatua isiyofaa, licha ya kukiri kuwa wana deni kubwa la kampuni hiyo.
“Kukatia gereza hili stima ni adhabu kubwa kwetu inayohatarisha usalama wa kila mmoja, hata kama tuna deni kubwa la kampuni hiyo. Tumeimarisha usalama,” alisema Mwenda.
Alitaka tatizo hilo kutatuliwa kwa maelewano ili shughuli za kawaida zirejelee.