Mbunge wa Nakuru mashariki David Gikaria ameomba msamaha kutokana na matamshi aliyotoa siku ya Jumapili juma lililopita ya kuhalalisha ukahaba, baada ya mwanamke mmoja anayesemekana kuwa kahaba kuuawa.
Akizungumza na wanahabari mjini nakuru Jumamosi ya tarehe 23 Januari, Gikaria alisema kuwa matamshi yake yalitokana na hasira aliyokuwa nayo kufuatia kifo cha mwanamke huyo.
Gikaria ambaye amekiri kuwa amelelewa katika maadili na muongozo wa kanisa katoliki aliongeza kuwa kuhalalisha ukahaba ni kwenda kinyume na dini hiyo, na kuwa ni kumkufuru mwenyezi mungu.
Aidha amesisitiza kuwa iwapo mswaada huo utapelekwa bungeni hataupigia upatu, badala yake atawarai wabunge wenzake wasiupitishe kwani utakuwa unaenda kinyume na maadili ya jamii.
Mbunge huyo ambaye amesema atatetea kiti hicho katika uchaguzi mkuu ujao aliongeza kuwa la muhimu ni kutafuta njia ya kuwasaidia ili waweze kuachana na biashara hiyo aliyoitaja kama ya aibu.
Kadhalika amewataka viongozi kutoka eneo hili kuwaita wanaodaiwa kufanya biashara ya ukahaba katika kikao na kuzungumza nao ili wapendekeze biashara au kazi zipi wanaweza kufanya ili waweze kuendeleza maisha yao.
Itazingatiwa kuwa takriban wanawake tisa wanaodaiwa kuwa makahaba wameuawa katika hali ya kutatanisha, jambo ambalo lililopelekea makahaba hao kufanya maandamano mara kadhaa mjini Nakuru na maeneo mengine humu nchini.
Haya yanajiri huku baadhi ya wabunge kutoka kaunti ya Nakuru, ikiwemo mbunge wa eneo bunge la Nakuru magharibi Samuel Arama wakitaka ukahaba uhalaliswe.