Balozi wa Marekani humu nchini Robert Godec amesema kuwa ushirikiano baina ya taifa la Marekani na Kenya utazidi kuimarishwa ili kuona kwamba masuala ya kiusalama yaangaziwa vyema hususan eneo la Pwani.
Akiongea na wanahabari baada ya kutembelea makavazi ya kitaifa ya Fort Jesus mjini Mombasa siku ya Jumanne, Godec alisema kuwa atahakikisha kuwa uhusiano bora unazidishwa baina ya wananchi wa Marekani, mashirika ya kijamii na wakazi wa eneo la Pwani ili kudhibiti usalama.
Godec amesema kuwa serikali za mataifa hayo mawili yako tayari kuhakikisha wananchi wako salama huku akisema kuwa iwapo usalama utaimarika basi sekta ya utalii itaboreshwa zaidi kwani serikali ya Marekani iko na imani na Kenya ndiposa ikaondoa marufuku ya Rais wao kutozuru Kenya.
"Serikali ya Marekani iko tayari kushirikiana na Kenya kuimarisha usalama na utalii hususan eneo la Pwani na tutahakikisha wageni na watalii wanazuru eneo hili kwa sababu mimi mwenyewe nimeona usalama uko Pwani na Mombasa pia," alisema Godec.
Naye Gavana wa kaunti ya Mombasa Ali Hassan Joho amesema kuwa amepongezwa ha hatua ya taifa la Marekani kupitia kwa Balozi huyo kuondoa marufuku hiyo ili kuimarisha uchumi sekta ya utalii ili kumbwa na changamoto huku akiahidi kushirikiana na ubalozi wa marekani humu nchini katika maswala ya kiusalama.
"Kama serikali ya kaunti ya Mombasa tunaunga mkono juhudi za Marekani kuondoa marufuku ya raia wao kutozuru Kenya hususan eneo la Pwani na Mombasa lakini sasa tunafurahi biashara na utalii utaimarika zaidi", alieza Joho.
Kwa upande wake Mbunge wa Mvita Abdul Sharrif Nassir amewataka wageni na watalii kuzuru katika mji wa Mombasa na kutalii sehemu mbalimbali ili kukuza utamaduni wa kipwani na sekta ya utalii.