Shirika la kutetea haki za binadamu la Haki Afrika limewahimiza wanajeshi wa KDF kuzingatia haki za binadamu katika operesheni yao nchini Somalia.
Mkurugenzi wa shirika hilo, Hussein Khalid, amewataka wanajeshi hao kutotumia nguvu kupita kiasi kimo cha kuwadhuluma wasio na hatia wanapofanya operesheni dhidi ya wanamgambo wa al-Shabaab.
Akizungumza afisini mwake mjini Mombasa siku ya Jumanne, mtetezi huyo wa haki za binadamu alisema kuwa anaunga mkono juhudi za jeshi la KDF kupambana na magaidi ila lazima haki za binadamu ziheshimiwe na zilindwe.
“Tunajua jeshi letu liko Somalia kudumisha amani lakini tusivunje haki za wengine wasio na makosa,” alisema Khalid.
Kauli ya Khalid inajiri huku wakaazi wa El Adde, Somalia, eneo ambalo jeshi la KDF lilishambuliwa na al-Shabaab, wakisema kuwa wanajeshi Wakenya wameanza kulihama eneo hilo.
Hata hivyo, msemaji wa jeshi la KDF kanali David Obonyo, amesema hatua ya wanejeshi hao kulihama eneo hilo ni la kawaida.