Idara ya usalama katika Kaunti ya Mombasa imetakiwa kuwapokonya wanaomiliki bunduki kinyume cha sheria bunduki hizo ili kupunguza visa vya uvamizi na mauaji yanayozidi kushuhudiwa jijini kila uchao.
Akizungumza siku ya Alhamisi, Francis Auma, afisa wa usalama katika shirika la utetezi wa haki za binadamu la Haki Afrika, alisema kuwa anaghadabishwa kuona jinsi majambazi wengi wanamiliki bunduki kinyume cha sheria, na hatimaye kuzitumia kuhangaisha wananchi wasiokuwa na hatia.
Kwenye kikao na mwanahabari huyu, Auma alisema kuwa wananchi na wafanyibiashara sasa wanaishi kwa hofu ya kushambuliwa na majambazi hao ikizingatiwa kuwa wao ndio walengwa.
Aidha, aliwataka wakazi kushirikiana na polisi kufichua majambazi wanaomiliki bunduki ili hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi yao.
Kauli hii inajiri baada ya dereva wa tuktuk kuuwawa kwa kupigwa risasi katika mzunguko wa barabara ya Jomo Kenyatta, eneo la Lebanon, karibu na Kanisa la Mombasa Pentecostal mjini Mombasa siku ya Jumatano.
Mauaji haya yanajiri wiki moja baada ya mfanyabiashara mmoja kupigwa risasi na kuuliwa katika mtaa wa Kisauni mjini Mombasa, huku dereva mwingine wa tuktuk akiuwawa kwa kudungwa kisu na kundi moja la vijana katika eneo la Bunley huko Majengo mjini Mombasa.