Share news tips with us here at Hivisasa

Wasiwasi kwa mara nyingine umeghubikia eneo la Maella mjini Naivasha baada ya watu wasiojulikana kujaribu kuchoma shule mbili za umma mapema Jumatatu.

Washukiwa hao aidha wamekata kwa kuchimba barabara mbili zinazoelekea eneo hilo huku masomo katika shule hizo yakitatizika na kubidi kufungwa.

Wakati wa tukio hilo, nyumba moja pia imeteketezwa huku wengi wakishindwa kuelekea eneo hilo kwani hata barabara zimefungwa.

Polisi wa kuzima ghasia wametumwa eneo hilo huku wanafunzi wote ambao walirejea shuleni Ijumaa wiki jana na hii leo (Jumatatu) wakirejea nyumbani.

Mkazi mmoja Jane Muthoni amesema kuwa baadhi ya familia sasa zinapania kuhama eneo hilo kwa hofu ya uvamizi.

Kulingana naye, wanaotekeleza maovu hayo wanalipiza kisasi kwa watu 25 waliotiwa mbaroni wiki jana na kufikishwa mahakamani ambapo walitozwa bondi za juu.

“Tunahofia mashambulizi sasa na tuna wasiwasi kuwa watu hao wanataka kulipiza kisasi kutokana na kutiwa mbaroni kwa waliohusika hapo awali,” alisema Bi Muthoni.

Mkuu wa tarafa ya Kongoni John Opondo amedhibitisha hali hiyo na kusema kuwa mavamizi hayo yalikuwa yamepangwa, huku akiongeza kuwa polisi wametumwa ili kuweka amani.