Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Hali ya utulivu imerejea katika eneo la Kosovo huko Ndabibi mjini Naivasha, siku moja tu baada ya mwanaume mmoja kuuawa na nyumba kadhaa kuteketezwa.

Wazee wa jamii za Kalenjin na Maasai wamearifiwa kuongoza shughuli za maridhiano ili wakazi waweze kurejelea shughuli zao za kawaida.

Haya yamejiri huku serikali ikionya kuwa yeyote atakayepatikana akiwachochea wakazi hao atachukuliwa hatua za kisheria.

Akitoa agizo hilo, mkuu mpya wa wilaya ya Naivasha, Isaac Masinde amesema kuwa baadhi ya viongozi wa kaunti ya Narok ndio wa kulaumiwa kwa uchochezi huo.

“Viongozi wa kaunti jirani ndio wamekuwa wakiwachochea wakaazi kupigana na tutawachukulia hatua baada ya kukamilisha uchunguzi wetu kama utawala wa mkoa,” alisema Masinde.

Mzozo huo unatokana na  umiliki wa shamba la ADC lenye ekari 2,000 ambapo kila upande wa jamii hizo wanadai umiliki.