Share news tips with us here at Hivisasa

Hali ya utulivu imerejea katika eneo tata la Maella mjini Naivasha huku polisi wakiwatia nguvuni washukiwa wanane akiwemo MCA wa eneo hilo kwa tuhuma za uchochezi.

MCA huyo Kariuki Mujina na baadhi ya wazee wengine walitiwa mbaroni Jumanne jioni huku wakidaiwa kuhusika pakubwa kuwachochea wakazi hao kuzua vurugu. Kikosi kikubwa cha maafisa wa polisi kilitumwa eneo hilo.

Mnamo Jumatatu wiki hii, zaidi ya wakazi 1000 wa eneo hilo walivamia ardhi zinazomilikiwa na wakurugenzi wa shamba la Ng’ati na kuharibu mali ya dhamani kubwa.

Na siku ya Jumanne wakazi hao walifika kwenye makaazi ya wakurugenzi hao na kuchoma nyumba saba, tukio lililowabidi polisi kuingilia na kuwatia mbaroni watu kumi na wanne.

Uuzaji wa ardhi yenye ekari 3,093 umeonekana kuwagadhabisha wakazi hao wanaosema kuwa njia halali haikufuatwa.

OCPD wa Naivasha Titus Munyoki amedhibitisha kisa hicho na kusema kuwa waliotiwa mbaroni watafikishwa mahakamani na kukabiliwa na makosa kadhaa huku akidhibitisha kuwa hali ya utulivu imerejea katika eneo hilo.

“Tayari tulishawakamata washukiwa wakuu katika ardhi hiyo na karibuni watafunguliwa mashtaka. Kwa upande wa usalama hali imerejea ya kawaida lakini bado polisi wanashika doria mpaka hali iwe nzuri kabisa,” Alisema Munyoki.