Wakulima wanaokuza zao la chai katika maeneo mengi kaunti ya Nyamira wamepata sababu ya kutabasamu baada ya halmshauri ya ukuzaji zao la chai nchini KTDA kutangaza mipango ya kufungua kiwanda kipya cha usagaji chai kule Matunua kwenye eneo wadi ya Gesima.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akihutubia wakazi wa eneo hilo  siku ya Jumanne, mwanakamati wa bodi ya KTDA Charles Achoki alisema kuwa kiwanda hicho kitagharimu shillingi millioni mia 700, huku akiongezea kuwa mwanakandarasi aliyepewa kandarasi hiyo ataanza kazi ya kujenga kiwanda hicho hivi karibuni. 

"Kama usimamizi wa KTDA tayari tumetenga shillingi millioni mia 700 kwa ujenzi wa kiwanda hiki na hivi karibuni mwanakandarasi atakayekuwa akijenga kiwanda hiki ataanza kazi mara moja kwa maana mikakati imewekwa kuhakikisha hilo linatimizwa," alisema Achoki. 

Achoki aidha aliongeza kusema kuwa kiwanda hicho kitasaidia pakubwa kurahisishia viwanda vingine kazi ya usagaji chai, huku akiongezea kuwa kiwanda hicho kitabuni nafasi za kazi kwa wenyeji. 

"Nina hakika kwamba sote tunajua umuhimu wa kiwanda kama hiki tunachotaka kukifungua hapa, na kwa hakika kuwepo kwa kiwanda hiki kitasaidia viwanda vingine kwa kurahizisha kazi na pia kitabuni nafasi za kazi kwa wenyeji wa eneo hili," aliongezea Achoki.