Shirika la kutetea haki za binadamu HURIA kwa ushirikiano na tume ya huduma za polisi nchini limeanzisha hamasa kuhusu shughuli ya uchuguzi wa maafisa wa usalama.
Kulingana na Kamishna wa Tume ya huduma kwa polisi Murshid Mohammed, hamasa hizo zimeanzishwa ili kukabili changamoto za ufisadi zinazotajwa kutatiza harakati za kudumisha usalama wa taifa.
Akizungumza kwenye warsha ya kuhamasisha wadau wa haki za binadamu mjini Mombasa siku ya Ijumaa Murshid alisema kwamba ni jukumu la wadau kuhakikisha kuwa wanawasilisha lalama zao kuhusu maafisa wasiowajibika au wafisadi.
Murshid, aidha alisema kuwa uaminifu katika masuala ya usalama ni kigezo muhimu, hivyo basi lazima idara zote za usalama ziwe na uaminifu hususan kwa jamii wakati wa kupokea ushahidi kuhusu uhalifu.
“Ni jukumu la maafisa wa usalama kudumisha usalama kwa wananchi kwa kuwa waaminifu na kazi zao ili kusitisha kuwepo kwa huduma duni na kuwasaidia wanachi kuwasilisha lalama zao,” alisema Murshid.
Kwa upande wake mkurugenzi mkuu wa shirika la kutetea haki za binadamu la HURIA Yusuf Lule Mwatsefu, alitaja vituo mbali mbali vya polisi vilivyo barabarani kuwa lazima vitambulike kiserikali ili kuepusha ongezeko la ufisadi.
Mwatsefu hata hivyo alisema kuwa wako katika mstari wa mbele kutetea haki za wananchi huku akiwahimiza wapwani wawasilishe lalama zao kuhusu visa vya utovu wa nidhamu katika idara za usalama.