Shinikizo la wazazi kutaka kupata wajukuu haraka kutoka kwa watoto wao limehusishwa na sababu inayopelekea wengi wa wapenzi kuishia katika mahusiano bila kufanya utafiti kumhusu wanaopendana.
Haya ni kwa mujibu wa mtaalamu wa maswala ya kindoa G.K wa Mungu ambaye anasisitiza kuwa kutomfahamu umpendaye katika mahusiano kumechangia talaka za kila mara katika ndoa za kileo.
"Wazazi wengi huishia kuwapatia watoto wao msukumo, wa eti mimi nataka wajukuu rika lako wako na watoto na wameolewa wewe bado unasubiri nini," alisema G.K.
Amesema shinikizo la wazazi kutia msukumo kwa mwanao kuoa au kuolewa imeishia kupelekea wengi kufanya maamuzi ya kujutia baadaye ambayo huwaacha kwenye njia panda kwenye ndoa.
Ameongezea kuwa sababu zingine za talaka ni kugundua kuwa matarajio kama vile ya kifedha hayatatimia.
Amependekeza wapendanao kuchukua muda wakichumbiana kabla ya kuamua kuoana ili kuimarisha ndoa za siku hizi.