Kufuatia makabiliano baina ya askari wa usalama wa kaunti ya Mombasa na wahudumu wa magari ya taksi maarufu kama Tuk Tuk siku ya Jumatano, wahudumu hao wameapa kuwa hawatatishwa kamwe katika juhudi zao za kupigania haki zao kutokana na dhuluma za uongozi wa serikali wa kaunti hiyo.
Wahudumu hao wamewalaumu askari wa kaunti kwa kutumia nguvu zao vibaya dhidi ya raia ambao wanakuwa na harakati za kupigania haki zao kupitia kwa maandamano na kutaja visa vya Jumatano kama vya kustajabisha.
Wahudumu hao, kupitia kwa mmoja wao Hassan Swaleh kwenye mahojiano siku ya Alhamisi walisema kuwa askari hao wamekuwa na mtindo wa kugeuka utaratibu na sheria za kuwaongoza hasa nyakati za kukabiliana na umma, huku akimtaka gavana wa Kaunti ya Mombasa kuwachukulia hatua baadhi ya maafisa hao ambao wamekuwa mara kwa mara wakigeuka sheria za kikazi.
“Tunapenda kufuata sheria kama mkenya yeyote yule, lakini si kuvamiwa na kushikwa tunapoandamana dhidi ya dhuluma, na sharti askari wa kaunti kurudi darasani kusoma jinsi ya kushughulika masuala ya raia wanaopigania haki zao,” alihoji mmoja wa wahudumu hao.
Wahudumu hao walikuwa wakishiriki kwenye maandamano siku ya Jumatano wakilalamikia kutohusishwa kwenye uundwaji wa utaratibu na sheria za trafiki na serikali ya Kaunti ya Mombasa.
Wahudumu wa tuktuk kwenye maandamano. Wamelalamikia kudhulumiwa na maafisa wa kaunti ya Mombasa walipokua wanaandamana siku ya Jumatano.