Baadhi ya wanachama wa chama cha kutetea maslahi ya walimu nchini tawi la Masaba wamepuuza hatua ya rais Kenyatta kuisihi tume ya uajiri wa walimu TSC na chama cha KNUT kutoa kesi mahakamani za malalamishi ya nyongeza ya mishahara kwa walimu. 

Share news tips with us here at Hivisasa

Kulingana na katibu mkuu wa chama hicho tawi la Masaba Meshack Ombongi ni kuwa kauli ya Rais Kenyatta kuisihi tume ya TSC kuwalipa walimu mishahara yao ya mwezi Septemba kamwe hawezi badili msimamo wa walimu kuhusiana na serikali, huku akiongeza kusema kuwa walimu watafanya mageuzi makubwa kwenye uongozi wa taifa hili kwa kuwa serikali ya Jubilee inatumia mahakama kukandamiza haki za walimu. 

"Nafikiri rais amechelewa sana kutoa kauli hiyo kwa kuwa amekuwa akitazama mahakama ikitukandamiza, na ni jambo la kushangaza kwamba baada ya wakati huo wote sasa anaweza itisha mkutano wa kujadiliana kuhusiana na  swala tata la nyongeza ya mishahara, na kwa kweli wanachama wetu huku wameamua kufanya mabadiliko makubwa kwenye uongozi wa taifa hili mwaka wa 2017," alisema Ombong'i.

Kwa upande wake naibu katibu wa chama cha Knut tawi la Masaba James Oteki alisuta kauli ya Rais Kenyatta, huku akisema kuwa ni maonyesho tu ya mahusiano mazuri na umma huku akisisitiza kuwa walimu wamechoshwa kuhujumiwa na serikali ya Jubilee. 

"Rais Kenyatta alikuwa na nguvu za kuamru tume ya TSC kutii agizo la mahakama ya viwanda, na kwa sababu hiyo anayoyafanya ni kudhihirisha mahusiano mazuri na umma, ata sasa walimu wa eneo hili wamejiandaa kuipinga serikali kwenye uchaguzi mkuu ujao," alisema Oteki.