Seneta wa kaunti ya Nyamira Mong'are Okong'o amejitokeza kupinga vikali mgao wa pesa ambazo serikali kuu inazopokeza kaunti mbalimbali nchini.
Akihutubia wanahabari nyumbani kwake baada ya hafla ya makumbusho ya mamaye mzazi Bethseba Okong'o, Mong'are alisema kuwa asilimia 15 ya pesa ambazo serikali za kaunti zinazopokea hazitoshi kufadhili miradi muhimu.
"Sisi Maseneta kamwe hatuwezi kubali mgao wa asilimia 15 wa mapato yakitaifa ambayo serikali kuu inapokeza serikali za kaunti kwa maana pesa hizo hazitoshi kufadhili miradi muhimu hasa ya huduma za matibabu na miundomisingi," alisema Mong'are.
Mong'are aidha aliwahimiza wananchi kuchukua hatua yakusajiliwa na tume ya uchaguzi IEBC kama wapiga kura ili iwe rahisi kwake yeye kutetea kaunti ya Nyamira kupokea mgao wakutosha kwa maana serikali kuu hupokeza kaunti pesa kulingana na idadi ya watu katika kaunti.
"Ili kupokea mgao wa pesa wakutosha kwenye kaunti zetu sharti tujisajili kwa wingi kama wapiga kura kwa maana serikali kuu hutumia takwimu hizo ili kubaini ni kaunti zipi zinazopokea mgao fulani wa pesa," aliongezea Mong'are.