Hazina ya ustawishaji maeneo bunge katika eneo bunge la Rongai imetakiwa kukarabati kituo cha polisi kwenye eneo la Lomolo A kwa lengo la kuimarisha usalama.
Wakizungumza na mwandishi huyu Jumamosi, wakazi wa eneo hilo wakiongozwa na Joseph Soi walisema kwamba tangia wapewe mashamba na serikali miaka minne iliyopita, walitenga mahala pa kujengea kituo hicho.
“Sisi kama wenyeji wa Rongai tuliamua tujitolee na tukatoa kipande cha ardhi ambacho tulipendekeza tujengewe kituo cha polisi maanake usalama hapa umedorora kabisa,” alisema Soi.
Walisema kuwa licha ya kupeleka pendekezo hilo kwa afisi ya CDF, bado hawajapata usaidizi wowote.
“Hatujaona chochote ambacho kimefanyika tangia wakati tulitoa ardhi hiyo, juhudi zetu zinaendelea kugonga mwamba na sasa tunataka kuona washikadau wakichukua hatua na kutusaidia,” alisema mkazi mwingine William Rono.
Wamelalama kwamba janga la uhalifu kwenye eneo hilo limeongezeka kwa kiwango kikubwa haswa siku za hivi karibuni.
Wamemtaka mbunge wao Raymond Moi kusikia kilio chao na kuwapa usaidizi wa haraka.