Kuna hofu ya mkurupuko wa maradhi ya kipindupindu katika kata ya Ndalani katika kaunti ndogo ya Yatta baada ya watu kumi kufikishwa katika hospitali ya Matuu Level Four wakiwa na dalili za ugonjwa huo.
Mwanahabari huyu, akizungumza na afisa mkuu katika wizara ya afya kaunti ya Machakos Jackson Nthanga alisema kuwa pia visa vitatu vya maradhi hayo vimeshuhudiwa katika hospitali ya Machakos Level Five na sampuli kadhaa zimepelekwa katika maabara ya kiserekali kwa uchunguzi zaidi.
"Katika eneo la Mamba kuna uwezekano wa mkurupuko wa maradhi hayo sababu watu wawili tayari wamedhibitishwa kuwa nao, huku sampuli za wengine zikipelekwa Nairobi katika maabara ya serikali kwa uchunguzi zaidi," alisema Nthanga.
Aidha Nthanga alisema wanasubiria majibu ya sampuli hizo siku ya Jumapili (leo) ili kujua hali kamili.
Aidaha, aliwaomba watu katika kaunti hiyo kuhakikisha usafi wa mwili na mazingira ili kuepuka ugonjwa huo.