Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Tatizo la ukosefu wa huduma bora katika kivuko cha feri cha Likoni kumechangia pakubwa umaskini na kudorora kwa sekta ya biashara.

Wakizungumza mjini Mombasa siku ya Ijumaa, wakazi wa eneo hilo wakiongozwa na Ali Sasabu wamesema kuwa shughuli za kibiashara na utalii katika eneo hilo zimedorora kwa asilimia kubwa ikilinganishwa na hapo awali kufuatia kuwepo kwa huduma duni za feri katika kivuko hicho.

Sasabu amesema kuwa iwapo huduma za feri katika eneo la Mtongwe zitarejeshwa basi kwa kiwango kikubwa sekta ya biashara, utalii na uchukuzi utaimarika hata zaidi.

Sasabu amewataka wasimamizi wakuu wa shirika la huduma za feri nchini kuwajibikia majukumu yao kikamilifu ili kupunguza msongamano wa magari na msukumano wa kila uchao unaoshughudiwa katika kivuko cha feri cha Likoni.

"Tunataka kuwaona wasimamizi wakuu wa huduma za feri hapa Likoni wakiwajibikia majukumu yao vyema sambamba na kurejesha upya kivuko cha feri cha Mtongwe ili kurahisisha shughuli za uchukuzi na kuboresha sekta ya biashara na utalii zinazokumbwa na changamoto," alisema Sasabu.

Tatizo la hudumu za feri limedumu kwa muda mrefu licha ya viongozi mbalimbali wa sekta ya uchukuzi na utalii kuingilia kati swala la kuboreshwa kwa huduma za feri.