Huduma za upasuaji katika Hospitali ya Coast General zinatarajiwa kuimarika baada ya daktari maarufu kutoka marekani kuzuru hospitali hiyo na kuahidi ushirikiano.
Dkt Amos Dare, ambaye ni mtaalam wa upasuaji alizuru hospitali hiyo siku ya Jumapili na kukagua wodi kadhaa kabla ya kufanya mazungumzo ya kina na madaktari.
Ziara hiyo iliyoandaliwa na usimamizi wa hospitali hiyo pamoja na wakfu wa Gavana wa Mombasa Hassan Joho Foundation ulilenga kufanya majadiliano kuhusu jinsi huduma za upasuaji zitakavyoimarishwa katika kaunti hiyo.
Dkt Dare aliahidi kusaidia hospitali hiyo katika huduma za upasuaji pamoja na kutoa mafunzo maalum kwa madaktari.
“Nafahamu kwamba madktari haswa wa upasuaji wanahitaji ujuzi wa hali ya juu katika shughuli hii na mimi natoa ahadi kwamba nitashirikiana na hospitali hii pamoja na serikali ya Mombasa kuhakikisha kuwa tunatoa huduma bora,” alisema Dkt Dare.
Kwa upande wake, Gavana wa Mombasa Hassan Joho alimpongeza daktari huyo na kusema kuwa ana imani ziara yake italeta manufaa kwa wakaazi.