Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Takwimu kutoka wizara ya afya nchini zinaonyesha kuwa idadi ya wanawake wanaojifungua katika vituo vya afya imeongezeka kwa asilimia 40 kutoka mwaka wa 2014 hadi 2015.

Wizara hiyo imesema kuwa kati ya mwaka 2014/2015 jumla ya wanawake zaidi ya milioni moja walijifungua katika vituo vya afya kutoka wanawake zaidi ya laki sita kati ya mwaka 2012/2013.

Akizungumza jijini Mombasa siku ya Ijumaa, Waziri wa afya Dkt Cleopa Mailu alisema kuwa idadi hiyo imeongezeka kutokana na huduma ya kujifungua bila malipo iliyowekwa na serikali.

Akizungumza baada ya kufunga kongamano la maafisa wa afya, Mailu alisema kuwa wizara yake imetoa vyandarua milioni sita vya kukinga mbu katika maeneo yanayokabiliwa na athari za ugonjwa wa malaria, ili kupunguza vifo vya watoto wadogo pamoja na wanawake waja wazito.

Waziri huyo alisema kuwa wizara yake itawaajiri wafanyikazi elfu saba ili kukabiliana na maradhi hayo humu nchini.