Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Idara ya afya katika serikali ya kaunti ya Nyamira imeanzisha mchakato wakufanya kampeni yakuhamasisha wakazi dhidi ya madhara yakupasha watoto wasichana tohara.

Akihutubu katika kijiji cha Nyabuya siku ya Jumapili wakati wa kuzindua kampeni hiyo, katibu wa afya kwenye kaunti hiyo Douglas Bosire aliwaonya wakazi wanao shikilia mila hizo potovu ambazo zimepitwa na wakati akisema kuwa kuna njia nyingi zakuwavusha watoto wasichana daraja la utu uzima pasina kuwapasha tohara.

"Ni vibaya kwa watu wetu kuendelea kuwapasha tohara watoto wasichana kwa kuwa tamaduni hiyo potovu huwaweka kwenye hatari nyingi hasa wakati wakujifungua. Ningependa kuwahimiza wazazi kukumbatia njia mbadala na kuasi tabia yakuwatahiri wasichana," alisema Bosire.

Bosire alihimiza utawala wa mikoa kushirikiana na wizara ya afya ili kuhakikisha kuwa tamaduni hiyo ya ukeketaji inadhibitiwa huku akisisitiza kuwa kampeni hiyo itasaidia pakubwa kupunguza visa vya ukeketaji katika eneo hilo.

"Mwezi wa disemba uko karibu na haitakuwa rahisi kwa wizara ya afya pekee kupambana na ukeketaji miongoni mwa jamii ya wakisii na ndio maana naomba utawala wa mikoa kushirikiana nasi kwa kuwatia mbaroni baadhi ya watu watakao patikana wakiendeleza utamaduni huo," aliongezea Bosire.