Share news tips with us here at Hivisasa

Idara ya afya ya umma mjini Nakuru imelaumu kampuni moja ya makonge kwa kuenea kwa kipindupindu kwenye mipaka wa Kaunti ya Baringo na Nakuru.

Mkuu wa Idara ya afya mjini Nakuru Samuel Kingori amedai kuwa usimamizi wa Patel Farm umewazuia maskwota walioko eneo la Mogotio kwa kujenga vyoo kufuatia agizo la mahakama lililowaamrisha maskwota hao watoke kwenye shamba hilo.

Akiongea na wanahabari kwenye ofisi yake siku ya Jumatano, Kingori alisema ukosefu wa vyoo umefanya maskwota hao kujisaidia kando ya mto Molo, jambo ambalo limechangia kuenea kwa kipindupindu katika maeneo hayo.

“Tulipata thibitisho kuwa ni kinyesi kinachosababisha kipidupindu kwenye maeneo haya baada ya kufanya uchunguzi wa maji kwenye maeneo ya Kwa Kiringa, Mogotio Bridge, Alphaga na Kampi Huru,” Kingori alisema.

“Wasimamisi wa shamba hilo wamekuwa wakiharibu vyoo vya maskwota hao kila wanapojenga, hali ilnayowafanya wajisaidie kwenye mto. Hii imekuwa changamoto kwa kuzuia kuenea kwa ugongjwa huu wa kindupindu,” King’ori alisema.

Mwezi uliopita, mtu mmoja alithibitishwa kufariki juu ya ugonjwa huo na wengine 20 walipelekwa hospitalini walikotibiwa baada ya kuzuka kwa kipindupindu kwenye maeneo hayo.