Share news tips with us here at Hivisasa

Viongozi katika Kaunti ya Mombasa bado wamezidi kuelekeza kidole cha lawama kwa idara simamizi ya shirika la huduma za feri kwa madai ya kuzembea kutokana na huduma duni katika kivuko hicho cha Likoni.

Haya yanajiri baada ya kuonekana kutopungua kwa mikasa ya hitilafu za kimitambo za mara kwa mara katika feri hizo.

Kulingana na Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Ali Joho, hali hiyo ni ya kutamausha ikizingatiwa kuwa kivuko hicho kinatumiwa na asilimia kubwa ya wakazi wa Mombasa, na kudorora kwa huduma za feri zinaregesha nyuma hatua za kuimarisha maendeleo na uchumi wa kaunti hii.

Joho aidha amedokeza kuwa kuna haja ya serikali ya kitaifa kuweka mikakati thabiti ya kukabiliana na changamoto hizo ambazo wakazi wanaotumia kivuko hicho wanakumbana nazo kila uchao.

Vuta ni kuvute bado inaendelea kushuhudiwa baina ya viongozi katika kaunti ya Mombasa, usimamizi wa shirika la feri nchini na serikali ya kitaifa, huku miongoni mwa viongozi kutoka kaunti ya Mombasa wakieleza kutamaushwa kwao na jinsi serikali ya kitaifa inavyoshughulikia swala hilo.

Haya yalidhihirika wazi katika siku ya kuadhimisha miaka 52 ya uhuru ambapo Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho alishauri serikali ya kitaifa kushirikiana na mataifa ya kigeni ili kujenga daraja katika eneo hilo la Likoni ili kutatua tatizo hilo la msongamano wa watu na magari wanaotumia feri.

“Serikali lazima iwajibike katika kutafuta suluhu ya kudumu katika kivuko hiki la sivyo nitahusisha mataifa mengine, kuongezwa kwa feri mpya haijaleta manufaa mpaka sasa,” alisema Joho.

Hivi karibuni kumekuwa na visa kadhaa vya usafiri kulemazwa na watalii kukosa safari zao za ndege huku wafanyibiashara wakilalamikia kuathirika kwa bidhaa zao kutokana na msongamano.

Itakumbukwa kuwa majuma kadhaa yaliyopita kamishina wa Kaunti ya Mombasa Nelson Marwa alipendekeza kubadilishwa kwa usimamizi wa shirika hilo ili kutafuta suluhu ya matatizo hayo katika kivuko hicho cha Likoni, ila pendekezo hilo halikupokelewa vyema na baadhi ya viongozi nchini.