Muungano wa vijana wa amani katika Kaunti ya Mombasa wameikosoa Idara ya Mahakama nchini kwa madai ya kushiriki ufisadi.
Vijana hao wamewataka mahakimu na majaji kujitenga na ufisadi ili kuwajibikia majukumu yao.
Wakiongozwa na kiongozi wa vijana katika eneo la Kisauni mjini Mombasa Maxwell Masai, vijana hao walidai kuwa hatua ya mahakama kuchukua muda mrefu kukamlisha kesi zilizoko mahakamani imechangiwa na ufisadi katika idara za mahakama.
Akizungumza na wanahabari katika eneo la Kisauni mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Masai alisema kuwa madai ya hivi majuzi kuwa jaji wa mahakama ya juu zaidi alihusika katika kashfa za ufisadi, yanaonyesha wazi jinsi idara ya mahakama ilivyokosa mpangilio.
Masai ameitaka jopo la uchunguzi lililobuniwa na Jaji mkuu nchini Dkt Willy Mutunga, kufanya uchunguzi wa kina na kutoa ripoti mwafaka dhidi ya madai yanayomkumba jaji wa mahakama ya juu zaidi Philip Tunoi.
Tunoi anadaiwa kuhusika katika kupokea rushwa ya shilingi milioni 200 kutoka kwa Gavana wa kaunti ya Nairobi Dkt Evan Kidero, ili kutupilia mbali kesi ya uchunguzi dhidi ya mpinzani wake.
“Tunataka kuona jopo lililobuniwa na jaji mkuu likifanya uchunguzi wa kina na kutoa ripoti mwafaka dhidi ya madai hayo,” alisema Masai.