Idara ya usalama Kaunti ya Mombasa imetakiwa kuboreshwa zaidi na kuwa kujizatiti katika kuzuia visa vya vifo vinavyozidi kushuhudiwa kila uchao.
Kauli hii inajiri baada ya dereva wa TukTuk kuuwawa kwa kupigwa risasi katika mzunguko wa barabara ya Jomo Kenyatta, eneo la Lebanon karibu na Kanisa la Mombasa Pentecostal mjini Mombasa Jumatano jioni.
Wakizungumza na mwanahabari huyu siku ya Jumatano baada ya kushudia tukio hili, wakaazi hao wa eneo la Lebanon wakiongozwa na Salimin Hussein walisema kuwa wanaishi kwa hofu ikizingatiwa kuwa visa vya uvamizi na mauwaji vinazidi kukithiri jijini humo.
Kulingana na waliyoshuhudia tukio hilo, watu wawili waliokuwa wameabiri pikipiki walifika eneo hilo na kumfyatulia risasi mara mbili kichwani dereva huyo na kumuua papo hapo kisha wakatoweka.
Haijabainika wazi kiini cha mauaji hayo, kwani genge hilo linalokisiwa kuwa la majambazi, hawakumuibia chochote dereva huyo.
Mwili wa mwendazazke umepelekwa katika hifadhi ya maiti katika hospitali kuu ya ukanda wa pwani.
Mauaji haya yanajiri wiki moja baada ya mfanyabiashara mmoja kupigwa risasi na kuuliwa katika mtaa wa Kisauni mjini Mombasa, huku dereva mwingine wa tuktuk akiuwawa kwa kudungwa kisu na kundi moja la vijana katika eneo la Bunley huko Majengo mjini Mombasa.